MWISHO WA DUNIA
Riwaya
Mawimbi ya dunia yanamyumbisha Chibago kama matete yayumbishwavyo na upepo. Kila anachokishika hakishikiki, na kila njia anayoifuata haimfikishi atakako. Jitihada zake zinapofika ukomo ndipo kudura zinaibuka, Msamaria anamshika mkono na shari zilikupwa na heri zikajaa.
Chibago ni chatu mwenye njaa kali, anaposhiba anageuka na kutishia kummeza mlishi wake. Anafanya visa na kufanikiwa kuchoropoka. Kuponea chupuchupu hakumfanyi akome, bali anasababisha matatizo huko alikokimbilia zaidi ya kule alikotoka.
Arobaini zake zinatimia, ananasa mtegoni na kila mtu anaamini mwisho wa Chibago umewadia, lakini katika hali wasiyoitegemea anafanikiwa kunasuka. Wakati Chibago na washirika wake wakiamini vita vimefika ukomo, Dube; mtu anayedhaniwa ni mgonjwa wa akili anavihuisha na kuanza upya. Vita dhidi ya kirusi ambacho kinaitafuna jamii yetu kimyakimya na kuiweka hatima ya dunia msalabani...