Mbinu Za Usimamizi Wa Wafanyakazi
Kitabu hiki ni kwa ajili yako wewe, au nyie, wamiiliki wa biashara ndogo au za kati. Yaani: wakandarasi, wasanii wa filamu na wanamuziki. Wengine ni wamiliki wa vituo vya afya, gereji, baa, hoteli, maduka, karakana, shule na hata vyuo binafsi, nakadhalika. Biashara ikianzishwa inatakiwa kusimamiwa. Mmiliki huku, mfanyakazi kule. Zipo biashara zilizokufa mapema. Sababu? Usimamizi mbovu, hasa wa wafanyakazi. Ukweli, wafanyabiashara wengi hawana ujuzi huu. Wengi hutumia hisia, ubabe na vitisho. Madhara yake ni migogoro, hujuma, na huduma mbovu, ambazo hufukuza wateja. Kitabu hiki kinatoa suluhisho la kadhia hii, ili biashara hizi ziendeshwe kwa mafanikio.
Mafanikio halisi ya taasisi, kampuni au biashara hayategemei pekee mtaji wa fedha, teknolojia au eneo zuri la biashara. La hasha! Mafanikio hujengwa juu msingi wa usimamizi bora wa rasilimali watu. Wafanyakazi ndio wanaobeba, na kutafsiri kwa vitendo dira, maadili na malengo ya shirika. Na kiongozi bora ni yule anayejenga watu, nao watu wakamjengea taasisi au biashara. Kitabu hiki kinalenga kumpa msomaji maarifa ya vitendo kuhusu namna sahihi ya kuajiri, kuongoza, kuendeleza na kusimamia wafanyakazi kwa ufanisi. Kupitia kitabu hiki; wajasiriamali, mameneja, wasimamizi wa rasilimali watu, wakuu wa taasisi, pamoja na yeyote anayehusika na uongozi wa watu, anapewa uwezo wa kujenga timu imara, yenye maadili na morali ya juu kazini.