NGUVU YA KUSHINDA DHAMBI
Nafsi ya Mwanadamu ni kama uwanja wa mapambano dhidi ya Nguvu kuu mbili, ambazo hushindana kila wakati kwenye ulimwengu wa ki-Roho. Watu wengi ulimwenguni wameyumba katika misimamo, maamuzi sahihi, na hata maendeleo ya maisha yao kiujumla na mwisho kuanguka Dhambini. Hii hutokana na wenyewe kufahamu au pasipo kufahamu kwamba ni Nguvu gani iliyo sahihi ya kumwongoza ili ashinde Dhambi na hata kuwa na mafanikio ya kimaisha. Kitabu hiki kimekufikia wewe sasa na watu wote ulimwengni, lengo ni kumfungua kila mmoja apate maarifa ya kutosha kuhusu Nguvu kuu mbili ambazo hushindana na kupambana kila wakati ndani ya nafsi ili kuyatawala maisha ya Mwanadamu. Nguvu ndiyo nishati ya Mtu/kitu ili jambo litokee, na pasipo nguvu hakuna chochote ambacho kinaweza kutokea kwa Mtu/kitu kwenye ulimwengu huu, hivyo nguvu ndiyo chanzo cha matokeo ya kila kitu unachokiona mbele ya macho yako popote ulipo duniani. Hata katika nafsi ya Mwanadamu, kutokana na mambo yote anayo yafanya kila siku maishani mwake, chanzo ni nguvu inayo tawala kwenye nafsi yake na kumwongoza maishani. Nguvu ya kushinda Dhambi, vikwazo, changamoto na hata kuwa na mafanikio kwenye maisha, ndiyo Nguvu kuu na ya pekee impasayo kumwongoza kila Mtu kwenye maisha yake. Ni mwisho sasa wa wewe kusitasita, kutangatanga, kuteseka dhambini, kuwa njia panda, au kukwama kwenye jambo lolote, maana maarifa yamekufikia ili uyatumie kuubadili mfumo mzima wa maisha yako katika ubora wake na viwango vya hali ya juu. (Wagalatia 3:22).
GOODLUCK KIRUMBI DANIEL; Mwandishi wa Kitabu hiki (Nguvu Ya Kushinda Dhambi), ameandaa Nakala hii kwa umakini kabisa chini ya maongozo na Uweza wa Roho Mtakatifu tangu mwanzo mpaka mwisho wa kitabu hiki.
Amejikita hasa katika kuelezea na kufafanua ni kwa jinsi gani Mwanadamu anaweza kutumikia Dhambi aidha kwa kujua au pasipo kujua, hali anatamani kuacha Dhambi lakini jitihada za kuacha zinafika kikomo na kujikuta anarudi dhambini kama mwanzo au hata na zaidi.
Ameeleza kuhusu namna ambavyo nafsi ya Mwanadamu hukumbana na nyakati tofauti tofauti dhidi ya nguvu mbili ambazo hushindana na kuvutana kila wakati na hata mwisho nguvu itakayo tawala nafsi hujidhihirisha matokeo yake katika ulimwengu huu wa damu na nyama.
Nguvu ambayo humvuta na kumfanya Mwanadamu atumikie dhambi ameelezea kwa kina, hata hivyo pia ameeleza Nguvu ya kushinda dhambi, vikwazo na hata changamoto zote za maisha na kuwa na mafanikio ki-Roho, kiuchumi, na jamii kiujumla.
Mwandishi ni Mwalimu na Mhamasishaji wa vijana na hata watu wote hususani katika masuala ya ki-Roho, Afya, na mbinu halali za Mafanikio katika Maisha.