JINSI YA KUIBUA UBUNIFU ULIO NDANI YAKO
Mbinu Za 30 Kibunifu Zilizothibitishwa
Dhahabu inavutia kwa sababu ya mwonekano wake na thamani
yake. Leo hii ukigundua kwamba kwenye
shamba lako kuna dhahabu basi utajiri
unakuwa umepiga hodi mlangoni kwako. Yaani ule usemi wa kulala masikini kuamka
tajiri unakuwa umetimia kwako. Nani asiyependa dhahabu igunduliwe kwenye shamba
lake? Ni nani huyo? Leo hii ninapoandika utangulizi wa kitabu hiki thamani ya
dhahabu kwenye soko la dunia ni dola za kimarekani 38,000. Ambazo ni sawa na
shilingi za kitanzania 86,723,600 (milioni themanini na sita laki saba ishirini
na tatu na mia sita)!! Hii ndio dhahabu.
Sasa hayo yote yalikuwa ni tisa, ila kumi ni kwamba dhahabu
kila mtu anaaweza kuitafuta na kuipata. Zipo kila sehemu. Na cha kushangaza
zaidi ni kwamba dhahabu hizi hapa zipo karibu yetu sana. Dhahabu hizi hapa
hatuzioni kwa sababu hatuzipi kipaumbele. Naam, dhahabu hizi zipo ndani yetu.
Kitabu hiki kimelenga katika kuhakikisha kwamba wewe
unatumia dhahabu hii ambayo unayo ndani yako kwa viwango vya juu sana.
Je, dhahabu inayozungumziwa hapa ni ipi? Ni ubunifu ulio
ndani yako. Na dhahabu hii inaweza kujitokeza kwa namna tofauti, inaweza kuwa
ni kipaji cha kuzaliwa nacho, inaweza kuwa ni ujuzi ulio nao, inaweza pia
kiwango chako cha elimu, hata biashsara unayoifanya.
Kama unaishi katika dunia hii basi nina hakika kwamba walau
kuna kitu kimojawapo ambacho unacho kati
ya hivyo hapo nilivyotaja hapo juu na unaweza kukimudu kwa viwango vya juu kama
utaamua. Ukweli ni kwamba una kitu na kama unaona kwamba hauna kipaji, ujuzi,
kisomo cha kiwango fulani basi hapo kaa ujifikirie tena. Hapo ndipo utagundua kwamba una kitu cha
kuanzia na kitu hiki ni kimojawapo kati ya vitu hivyo hapo juu.
Sasa ukishajua kwamba upo wapi ndipo kitabu hiki hapa
kinaingillia kati kwa kukutaka wewe uibue ubunifu wako zaidi ya hapo. Kitabu
hiki hapa kinakutaka wewe hapo uweze kuupeleka ubunifu wako kwenye viwango
vingine tofauti na sasa.
Usifanye kitu kwa sababu tu unafanya, bali ufanye kazi kwa
kuongeza thamani zaidi kupitia ubunifu. Tumeona dhahabu unavutia watu walio
wengi kwa sababu ya mwonekano wake, basi na wewe utawavutia watu wengi zaidi
kwa kutumia ubunifu ulio ndani yako.