
KUMTUNZA MZEE MGONJWA NYUMBANI: MWONGOZO KWA FAMILIA
Uzee ni Baraka kumtunza mzee ni heshima, thawabu na jukumu la upendo.
Katika jamii nyingi, wazee ni hazina ya hekima, kumbukumbu, na msingi wa malezi bora kwa vizazi vijavyo. Hata hivyo, kadri wanavyozeeka, miili yao hudhoofika na mara nyingine huanza kukumbwa na magonjwa ya muda mrefu kama vile shinikizo la damu, kisukari, au udhaifu wa viungo mbalimbali. Wakati mwingine, hali zao\r\nhuwalazimu kupata msaada wa karibu kutoka kwa familia ili waweze kuishi kwa heshima, upendo na faraja.
Kitabu hiki, Kumtunza Mzee Mgonjwa Nyumbani: Mwongozo kwa Familia, kimeandaliwa kwa lengo la kuwasaidia wanafamilia na walezi kutoa huduma bora na yenye utu kwa wazee wagonjwa katika mazingira ya nyumbani. Kimekusudia kuwajengea uelewa juu ya mahitaji ya kiafya, kihisia na kijamii ya wazee, na kuwapa mbinu rahisi za kuwahudumia bila mzigo mkubwa wa kifedha au kiakili.
Katika mwongozo huu, utajifunza kuhusu:
Utunzaji wa kila siku wa mzee mgonjwa (chakula, usafi, mavazi).
Kushughulikia magonjwa ya mara kwa mara kwa wazee.
Namna ya kushirikiana kama familia na kugawana majukumu.
Mbinu za kuonyesha upendo, heshima na uvumilivu.
Jinsi ya kutafuta msaada kutoka kwa jamii au wataalamu wa afya.
Nimeandika kwa lugha rahisi, yenye mfano hai na picha panapohitajika, ili kila mshiriki wa familia kuanzia kijana hadi mtu mzima – aweze kuelewa na kushiriki kikamilifu katika huduma hii ya kipekee.
Ninatumaini kuwa mwongozo huu utakuwa msaada mkubwa katika kuimarisha maisha ya wazee wetu,na kuendeleza utamaduni wa kuwathamini na kuwajali hadi mwisho wa safari yao ya maisha.